Bobi Wine asema vitisho dhidi yake vimeongezeka
31 Julai 2025Kwenye mahojiano na shirika la habari la AP kwenye makao makuu ya chama chake cha National Unity Platform, mjini Kampala, Bobi Wine amesema kumekuwa na vitisho dhidi ya maisha yake na wanaharakati wengine wanaohamasisha upinzani dhidi ya rais aliyekaa muda mrefu nchini humo Yoweri Museveni.
"Hali imezidi kuwa mbaya zaidi kwa kila upande — vitisho dhidi ya maisha yangu vimeongezeka, pamoja na utekaji nyara, kukamatwa kwa watu, na hata mauaji. Kwa mfano, kaka mmoja huko Karamoja alipigwa risasi zaidi ya 150. Lengo ni kuwatisha wale wanaoshirikiana nami na wanaoamini katika misimamo yangu. Lakini badala yake, upinzani wetu umeimarika: wanachama wameongezeka, watu wanazungumza zaidi, na dhamira yetu imekuwa thabiti zaidi."
Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulani Ssentamu amesema kama mpinzani mkubwa wa Museveni, amekuwa na wasiwasi unaozidi kuongezeka katika kipindi cha karibuni, unaochochewa zaidi na mashambulizi kutoka kwa mtoto wa Museveni na Mkuu wa Majeshi Muhoozi Kainerugaba kupitia mtandao wa X.
Wasiwasi wachochewa zaidi na Mkuu wa Majeshi, Kainerugaba
Mwezi Januari, Kainerugaba aliandika kwamba atamkata kichwa Wine ikiwa rais atamruhusu kufanya hivyo. Na kama haitoshi, mwezi Mei alitoa matamshi yaliyoibua ukosoaji mkubwa aliposema alikuwa akimshikilia mlinzi wa Wine, ambaye alikuwa amepotea. Mlinzi huyo siku chache baadae alionekana akiwa mahakamani lakini akiwa hawezi kutembea bila ya kusaidiwa.
Amesema "Ni ukumbusho wa kila mara kwamba tishio hili ni la kweli, kwa sababu huyu si mtu wa kawaida. Ni mtoto wa kiongozi mkuu wa nchi na pia ndiye anayesimamia vyombo vyote vyenye nguvu — anasimamia jeshi, polisi, magereza — kwa kifupi, yuko juu ya sheria, na ameonesha wazi tabia hiyo. Amewateka watu wangu, akiwemo mlinzi wangu binafsi, akamfungia kwenye chumba cha chini ya ardhi, akampiga, akamvua nguo, akamnyoa, akampiga picha akiwa uchi na kuzisambaza mitandaoni."
Bobi Wine alidai kuibiwa kura mwaka 2021
Kwenye uchaguzi mwa mwaka 2021, Wine alipata asilimia 35 ya kura na Museveni alipata asilimia 58, matokeo yaliyotajwa kuwa mabaya kabisa kwa kiongozi huyo lakini yakimuonyesha dhahiri Wine kuwa mpinzani mkubwa wa Museveni baada ya miongo kadhaa. Wine lakini hakukubaliana na matokeo hayo akisema aliibiwa kura, ingawa Mamlaka za uchaguzi zilipinga madai hayo.
Viongozi hawa wawili wanakutana tena kwenye uchaguzi wa urais ulioapangwa kufanyika Januari 2026. Museveni tayari ameanza kampeni katika siku za karibuni mjini Kampala akijaribu kuimarisha nafasi yake miongoni mwa watu ambao pengine wanamuunga mkono Wine, hasa wale wenye kipato cha chini na wenye matamanio ya mabadiliko kupitia serikali mpya.
Wine ameiambia AP kuwa amekuwa akiwahamasisha wafuasi wake kujitokeza kuandamana kupinga kila kitu anachoamini kinafanywa kinyume na serikali, lakini majaribio yake ya kufanya mikutano nchini humo mara nyingi yamekuwa yakizuiwa na vikosi vya usalama ambavyo husema vinalinda utulivu wa umma.
Huku hayo yakiendelea, Kainerugaba ambaye pia ameonyesha nia ya kuwania urais nchini humo anazidisha hofu ya utawala wa kifamilia katika nchi ambayo haijawahi kushuhudia mabadilishano ya amani ya mamlaka tangu ilipopata uhuru mwaka 1962.
Museveni ameitawala Uganda tangu 1986, na anamtangaza Wine kama wakala wa maslahi ya kigeni na hata kutilia shaka uzalendo wake. Lakini Wine anakanusha madai hayo, ana ufuasi mkubwa miongoni mwa watu wa tabaka la wafanyakazi katika maeneo ya mijini na chama chake ndicho chenye viti vingi zaidi ya chama chochote cha upinzani katika Bunge la Uganda.