Blatter na Platini warejea mahakamani kwa kesi ya ulaghai
4 Machi 2025Blatter na Platini ambaye alikuwa rais wa shirikisho la kandanda Ulaya - UEFA, walirejea katika mahakama ya shirikisho karibu miaka mitatu baada ya kuachiliwa katika kesi ya kwanza Julai 2022 kwa mashitaka ya ulaghai, kughushi nyaraka na matumizi mabaya ya fedha za FIFA. Waendesha mashitaka wa Uswisi walikata rufaa kupinga hukumu hizo.
Blatter mwenye umri wa miaka 88 aliidhinisha malipo ya FIFA ya dola milioni 2.21 kwa nguli wa soka wa la Ufaransa Platini mnamo mwaka wa 2011 kwa kazi ya zamani wakati akiwa mshauri wa rais muongo mmoja kabla.Blatter na Platini wanakanusha kufanya kosa lolote katika kesi hiyo ambayo iko katika mwaka wake wa 10 na ambayo ilizimaliza taaluma za kisiasa za watu hao wawili waliokuwa na ushawishi mkubwa kabisa katika soka la ulimwengu.