Bilioni 11 zapotea kupitia mfumo wa e-Citizen Kenya
6 Agosti 2025Ripoti maalum ya ukaguzi imeonesha mapungufu makubwa kwenye uendeshaji wa mfumo wa malipo wa serikali wa e-Citizen na kuwepo kwa watu wasiojulikana wanaonufaika kimya kimya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takribani shilingi bilioni 7 za Kenya zilizokusanywa kutoka kwa wananchi zinashikiliwa na kampuni inayoendesha e-Citizen, pesa ambazo Mdhibiti Mkuu anaonya huenda zinatumiwa kinyume cha sheria, badala ya kuwasaidia wananchi kwa huduma za serikali.
Ripoti hiyo imeongezea kusema kuwa shilingi bilioni 2.5 hazijulikani zilipo kabisa. Ripoti hiyo inaeleza kuwa pesa hizo zilipotea kutokana na kurudiwa kwa malipo na makosa ya kiufundi, jambo linaloashiria kuwa mfumo huo haueleweki vizuri na uko wazi kwa wizi na ulaghai. Cha kushtua zaidi ni kwamba shilingi milioni 127 zilitolewa kwa watu binafsi katika siku moja tu, mnamo Januari 25, 2024, kupitia miamala minne ya kutatanisha, bila ruhusa wala ufuatiliaji wowote.
Isaac Ng'ang'a, naibu Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anazungumzia kuhusu kampuni ya Wandambwa na washirika wake na kampuni ya Gulro ambazo zilipokea pesa hizo.
''Kampuni mbili binafsi zilizolipwa shilingi milioni 127, zilikuwa za Wandabwa na washirika wake, shilingi milioni 63 na kampuni ya Gulro, pia shilingi milioni 63, pesa hizo zilikuwa sawa'', alisema Ng'ang'a.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa serikali iliwatoza wananchi zaidi ya shilingi bilioni 1.8 kwa makosa, kwa sababu haikutumia asilimia inayotakiwa kwenye ada za huduma.
"Jukwaa la mfumo huu wa e-citizen halifai kuendelea kuendeshwa"
Badala yake, ada ya shilingi 50 kwa kila muamala ilitumika, jambo lililoongeza gharama kwa wananchi bila sababu. Licha ya madai kuwa serikali inamiliki kikamilifu e-Citizen, ripoti hiyo inasema mfumo huo bado unaendeshwa na kampuni ya Webmasters Kenya Ltd, hali inayozua hofu kuhusu usalama wa data binafsi za wananchi.
Kinachoibua hasira zaidi kwa wananchi si tu upotevu wa pesa hizo, bali ni kimya kizito cha Rais William Ruto, ambaye amekuwa akijitambulisha kama kinara wa maendeleo ya kidijitali na anayepambana na ufisadi.
Tangu taarifa hizi kufichuka bungeni, Rais Ruto hajasema lolote, jambo linalozidi kutonesha kidonda cha kutoaminiana kwa wananchi na serikali. Tindi Mwale ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabau Bungeni.
''Naomba tuwe wakweli Wakenya, jukwaa la mfumo huu wa e-citizen, hauifai kuendelea kuendeshwa, kutokana na matokeo ya ripoti hii ya ukaguzi, na huo ndio ukweli.''
Haya yote yanajiri wakati mamilioni ya Wakenya wanakabiliwa na maisha magumu, kukosa ajira, na kutozwa kodi kila pembe, huku serikali ikishindwa kueleza mabilioni yanayopotea kupitia mfumo wake.
Maswali ambayo wananchi wanajiuliza ni nani anaendesha e-Citizen? Nani anayenufaika na mabilioni ya fedha zilizopotea? Nani atawajibika kwa usaliti huu mkubwa dhidi ya raia wa kawaida?
Na muhimu zaidi, nani atamtetea Mkenya wa kawaida, anayekamuliwa na kuvutwa chini kwa kodi, lakini sasa anaibiwa na mfumo uleule wa serikali?