Besigye ashtakiwa kwa uhaini unaobeba hukumu ya kifo
21 Februari 2025Besigye alisomewa mashtaka hayo ya uhaini akiwa na mshiriki wake Obed Lutale pamoja na mwanajeshi mmoja.
Hakimu amewasomea jumla ya mashtaka matatu ikiwemo kupatikana na bastola mbili na risasi.
Aidha wamedaiwa kufanya mikutano ya kuomba misaada ya kifedha huko Geneva, Ugiriki na Kenya.
Tangu kukamatwa kwa wawili hao mjini Nairobi mwezi Novemba mwaka jana, kumekuwepo mivutano ya kisheria na kisiasa hasa walipofikishwa katika mahakama ya kijeshi.
Uganda: Besigye afikishwa katika mahakama ya kiraia
Licha ya mahakama ya juu kuamua mwezi Januari kwamba mahakama ya kijeshi haina mamlaka ya kuwashtaki raia, washtakiwa hao wamendelea kuzuiliwa.
Kumekuwepo shinikizo waachiliwe kutoka ndani na nje ya nchi huku makundi ya wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani wakitisha kufanya maandamano kudai kuachiliwa kwao. Hili ni kutokana na kudhoofika kwa afya ya Besigye baada ya kuanza mgomo wa kula siku kumi zilizopita.