BERLIN:Ujerumani yaitaka Iran kuvuta subira na kurejea katika mazungumzo ya nuklia.
21 Septemba 2005Ujerumani imeishauri Iran kutochukua uamuzi wowote wa haraka na kuitaka nchi hiyo kurejea katika meza ya mazungumzo kuhusiana na mikakati yake ya nuklia.Hatua hiyo ya Ujerumani imekuja baada ya serikali ya Tehran kueleza kuwa haitoruhusu tena kufanyiwa ukaguzi wa ghafla katika vinu vyake vya nuklia,iwapo suala hilo litapelekwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Msuluhishi mkuu katika mazungumzo ya nuklia kwa upande wa Iran,Ali Larijani amesema Iran pia itafikiria kujiondoa katika mkataba unaopiga marufuku uenezaji wa nuklia.
Kwa upande wao Marekani na Umoja wa Ulaya wanataka kuipeleka Iran mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,ili nchi hiyo ichukuliwe hatua za kuwekewa vikwazo,iwapo itashindwa kutoa ushirikiano unaotakiwa kwa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa.
Iran ambayo mwezi uliopita ilianza tena shuguli zake za kurutubisha madini ya uranium yanayotumika kutengenezea nuklia,imezidi kusisitiza kuwa shughuli hizo ni kwa ajili ya masuala ya amani peke yake na sio kutengenezea silaha za nuklia.