BERLIN:Nani atakuwa Kansela mpya wa Ujerumani labakia kuwa suala zito
7 Oktoba 2005Mazungumzo kati ya Kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder wa chama cha SPD na kiongozi wa CDU Angela Merkel juu ya nani anayefaa kuwa kansella mpya hapo jana yalimalizika bila kupatikana jawabu.
Hakuna kati ya vigogo hao wawili wa kisiasa Schröder wala Merkel aliyezungumza na waandishi habari kufuatia mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na kiongozi wa SPD Franz Münterfering na Edmund Stöiber wa chama cha CSU.
Kufuatia mazungumzo hayo hata hivyo pande zote mbili SPD na CDU zimesema hakuna uamuzi utakaofikiwa juu ya nani atakawa Kansella mpya wa Ujerumani hadi pengine jumapili.
Viongozi wote wawili Schröder na Merkel wanadai kuwa na haki ya kuiongoza Ujerumani kufuatia uchaguzi uliopita ambapo chama cha CDU kilijizolea ushindi wa viti vinne zaidi ya SPD.