BERLIN:Mkutano wa Afghanistan kufanyika Ujerumani
8 Desemba 2003Mkutano mpya juu ya mustakbali wa Afghanistan baada ya uchaguzi wa mwaka 2004 unajadiliwa katika ngazi ya kimataifa na yumkini ukafanyika nchini Ujerumani hapo mwakani. Msemaji wa kike wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amesema mkutano huo ambao utakuwa wa tatu katika mfululizo wa kile kinachojulikana kama mikutano ya Petersberg iliokuwa ikifanyika hapa Bonn mji wa magharibi wa Ujerumani utabidi ukubaliwe na washiriki wa mikutano iliopita ili uweze kufanyika. Lakini amesema nadhari hivi sasa imelekezwa kwenye loya jirga baraza kuu la Afghanistan ambalo linakutana nchini humo hapo kesho na ambalo litajadili na kuidhinisha katiba mpya ambayo itaanzisha mfumo madhubuti wa serikali itakayoongozwa na Rais. TEHRAN:Watalii wa Ujerumani na Muirish watekwa Wafanya biashara ya madawa ya kulevya wamewateka nyara watalii wawili wa Kijerumani na mmoja wa Ireland wakiwa katika safari ya matembezi ya baiskeli kusini mashariki mwa Iran na wamedai kulipwa euro milioni tano za kuwagombolea ili waachiliwe huru. Duru za serikali ya Iran ambazo zimekataa kutajwa jina zimeliambia shirika la habari la Uingereza Reuters leo hii kwamba tukio hilo la utekaji nyara limetokea wiki iliopita katika jimbo la Sista Baluchistan lilioko karibu na mipaka ya Afghanistan na Pakistan.Amesema watalii hao walitekwa na wafanya biashara hao wa magendo wakati wakiwa katika barabara kati ya miji ya Bam na Zahedan. Duru hizo zimekataa kusema hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha watalii hao wanaachiliwa.