BERLIN:Kampeini za Uchaguzi wa Ujerumani zashika kasi
17 Septemba 2005Wanasiasa wa hapa Ujerumani wametupilia mbali utaratibu wao wa zamani na badala yake wanaendelea na kampeini ya uchaguzi hadi hapo kesho Jumapili siku ya uchaguzi wenyewe.
Kupamba moto huko kwa kampeini ya uchaguzi kumekuja huku uchunguzi wa maoni ukionyesha kuwa asilimia 25 ya wapiga kura bado hawajaamua ni yupi wa kumpigia kura kati ya vigogo wawili wa kisiasa Kansela Gerhard Schroder au Angela Merkel.
Kwa mujibu wa uchunguzi tofauti uliotolewa hivi punde unaonyesha kuwa chama cha kihafidhina cha CDU pamoja na washirika wao inachopendelea kuunda nao serikali ya mseto chama cha kiliberali cha Demokrat vinaweza kujipatia ushindi wa viti vichache bungeni.
Kansela Gerhard Schroder alianza kampeini yake ya mwisho mwisho hapo jana kwa kufanya mkutano wa hadhara mjini Berlin ambapo ameishutumu mipango ya mageuzi ya kiuchumi ya CDU kwa kusema kwamba itakuja kusabisha mgawanyiko mkubwa katika jamii kati ya wanaojiweza kimali na walala hoi.
Mpinzani wa Kansela, wa CDU Angela Merkel naye naye pia katika kampeini yake Mjini Berlin ameuwambia mkutano wahadhara wa chama chake kwamba serikali ya Kansela Shroder ya mseto ya mlengo wa shoto wa wastani imeshindwa kutimiza ahadi zake tokea iingie madarakani miaka saba iliyopita.