BERLIN: waziri wa zamani ajitetea katika kashfa ya Visa.
22 Aprili 2005Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Ujerumani Ludger Volmer amekanusha shutuma zilizotolewa na upinzani kuhusu ulegevu wa sheria za utoaji wa visa za Ujerumani wakati alipokuwa mamlakani na kusababisha kuingia kwa wingi nchini Ujeruamani wahalifu kutoka mataifa ya ulaya mashariki.
Akitoa ushahidi wake mbele ya jopo la wanabunge Volmer alisema kuwa alitoa agizo la kulainisha sheria za utoaji visa katika balozi za ulaya mashariki kwa misingi ya kibinadamu.
Wanasiasa wa chama cha kijani wanasema kuwa agizo hilo lilitaka familia zipate nafasi ya kutembeleana kwa urahisi na ni hatua ambayo ilipitishwa kwa makubaliano ya vyama vyote miaka mitano iliyopita.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Joschka Fischer anatarajiwa kufika mbele ya jopo hilo la wanabunge siku ya jumatatu.