Berlin. Waziri wa mambo ya kigeni nchini Ujerumani ahojiwa kwa saa 12 kuhusiana na kashfa ya visa.
26 Aprili 2005Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Bwana Joschka Fischer ameondoa uwezekano wa yeye kujiuzulu kuhusiana na kile ambacho kinajulikana nchini Ujerumani kama kashfa ya visa.
Lakini wakati huo huo , amekiri kufanya makosa na amechukua jukumu la kisiasa kitokana na hayo.
Haya yamekuja wakati Bwana Fischer akitoa ushahidi wake katika uchunguzi wa bunge kuhusiana na kashfa hiyo, uliotangazwa moja kwa moja katika televisheni .
Chama cha upinzani cha kihafidhina cha Christian Democratic Union kimesema kuwa hatua ya kulegeza masharti ya viza ambayo wizara hiyo ilianzisha , imepelekea kuwa rahisi kwa makundi ya wahalifu kuwaingiza wahamiaji haramu nchini Ujerumani kutoka mataifa ya Ulaya ya mashariki.
Katika muda wa saa 12 za kutoa ushahidi wake , Bwana Fischer pia ameushutumu upande wa wapinzani kwa kulikuza tatizo hilo kwa sababu ya kujipatia maslahi ya kisiasa.