Berlin. Wataalamu wa Ujerumani waenda New Orleans.
10 Septemba 2005Kundi la wataalamu kutoka Ujerumani wanatarajiwa kujiunga na juhudi za kuondoa maji katika mji wa New Orleans ulioathirika na kimbunga Katrina .
Wataalamu hao 94 kutoka katika kitengo cha wataalamu wa uokozi katika serikali ya shirikisho la Ujerumani waliwasili jana usiku wakiwa na vifaa 15 vya kuvuta maji na kuongeza idadi ya vifaa vilivyopo hivi sasa katika kazi ya kuondoa maji ya mafuriko katika mji huo.
Wakati huo huo baada ya siku kadha za malalamiko na ukosoaji kuwa rais George W . Bush na kundi lake la viongozi wameshindwa kuchukua hatua za haraka na za kutosha kuwasaidia wahanga wa kimbunga Katrina , kiongozi wa idara ya kutoa misaada ya dharura ya serikali ya Marekani Michael Brown ameitwa mjini Washington.
Nafasi ya Bwana Brown inachukuliwa na mkuu wa kanda wa masuala ya uokozi katika jeshi la ulinzi wa pwani ya nchi hiyo Thad Allen.