BERLIN : Wahafidhina washinikiza kuwania Ukansela
30 Septemba 2005Chama cha wahafidhina CDU nchini Ujerumani kinashinikiza kupatikana kwa uamuzi wa nani atakayekuwa Kansela mpya ifikapo wiki ijayo.
Kiongozi wa chama cha Kisoshalisti SPD Franz Muntefering amekanusha kwamba Kansela wa hivi sasa Gerhard Schroeder anapanga kutanguwa azma yake ya kuwania wadhifa huo hapo Jumatatu wakati wa sherehe za Siku ya Muungano wa Ujerumani. Iwapo mazungumzo kati ya CDU na SPD juu ya kile kinachojulikana kama serikali ya mseto ya muungano mkuu yatashindwa kufanikiwa wahafidhina wametamka bayana kwamba wako tayari kuanza tena mazungumzo na vyama viwili vidogo kile cha kiliberali cha FDP na cha mazingira cha Kijani juu ya kuunda serikali ya mseto ya vyama vitatu.
Mazungumzo mengine kati ya vyama hivyo vikuu vya CDU na SPD yanatazamiwa kufanyika tena hapo Jumaatano.