BERLIN : Wagombea kupiga kampeni mpaka dakika za mwisho
16 Septemba 2005Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani na mpinzani wake wa kihafidhina Angela Merkel waapa kuondokana na mtindo wa asili na badala yake kuendelea kuwania kura za mwisho kabisa hadi pale vituo vya uchaguzi vitakapofungwa wakati Ujerumani ikijiandaa na uchaguzi huo mkuu wa Jumapili unaotazamiwa kuwa wa mchuano mkali.
Ikiwa inaongoza kwa poiti 7 hadi 9 dhidi ya SPD chama cha mrengo wa shoto wa wastani cha Shroeder chama cha CDU inaonekana kina uhakika wa kuwa chama kikubwa kabisa bungeni na kumfanya Merkel kuwa kansela wa kwanza mwanamke nchini Ujerumani.
Ili kuhakikisha hatamu huru ya kupitisha mageuzi magumu ya kiuchumi ambayo mwananama huyo anatumai kuwa yatafufuwa uchumi iliozorota wa Ujerumani Merkel amesema anahitaji kuunda serikali ya mseto na chama cha kiliberali cha FDP.
Bado haiko bayana iwapo ataweza kuunda serikali hiyo au badala yake kulazimika kuunda serikali ya muungano mkuu na chama cha SPD cha Schroeder ambacho hakikubaliani na mipango mingi ya chama chake.
Kinyume na utaratibu wa kawaida Schroeder na Merkel wameahidi kuendelea na kampeni hadi pale upigaji kura utakapomalizika saa kumi na mbili jioni.
Matokeo ya mwisho ya uchunguzi wa maoni yanatarajiwa kutolewa baadae leo hii.