Berlin. Vyama vinavyounda serikali ya mseto vinataka kupunguza deni la taifa.
26 Oktoba 2005Chama cha Christian Democratic Union na cha Social Democrats vinafikiria kuchukua hatua ngumu zenye lengo la kupambana na deni la ndani nchini Ujerumani.
Kufuatia duru ya pili ya mazungumzo mjini Berlin yenye lengo la kuunda serikali ya mseto katika kile kinachofahamika kama muungano mkuu, pande zote mbili zimesema kuwa zinataka kupunguza matumizi ya serikali kwa kiasi cha Euro 35 bilioni ifikapo mwaka 2007.
Hii wamesema , inairejesha Ujerumani chini ya kiwango cha kawaida cha umoja wa Ulaya cha nakisi katika matumizi ya umma yanayofikia asilimia tatu ya pato jumla la taifa.
Ujerumani imekiuka kiwango hicho kwa muda wa miaka michache iliyopita. Miongoni mwa hatua hizo zinazofikiriwa ni pamoja na ongezeko la kodi ya nyongeza ya thamani na kupunguza ruzuku kwa watu wanaomiliki nyumba.
Pande hizo mbili zinamatumaini ya kukamilisha makubaliano ya kuunda muungano katika muda wa wiki tatu zijazo.