BERLIN: Ulaya yakumbuka mwisho wa Vita Vikuu vya Pili
9 Mei 2005
Sherehe za kumbukumbu zimefanywa kote Ulaya kuadhimisha mwaka wa 60 tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.Katika miji ya Berlin,London,Paris na kwengineko viongozi walikusanyika kuwaheshimu wale waliofariki vitani kati ya mwaka 1939 na 1945.Wakati wa vita hivyo,hadi watu milioni 60 walifariki kote duniani.Rais George W.Bush wa Marekani nchini Uholanzi,aliongoza sherehe ya kumbukumbu kwenye makaburi ya Marekani karibu na mji wa Maastricht.Takriban wanajeshi 8,000 wa Marekani waliokufa katika Vita Vikuu vya Pili wamezikwa huko.Na mjini Berlin,rais wa Ujerumani Horst Köhler na Kansela Gerhard Schroeder waliweka mashada ya maua kuwakumbuka mamilioni waliouawa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.Rais Köhler alisema Ujerumani kwa aibu inayatazama mateso iliyosababisha na kamwe Ujerumani isisahau historia yake.