BERLIN Ujerumani yaziongezea nguvu sheria za mikutano ya hadhara.
23 Februari 2005Serikali ya Ujerumani imeamua kuziongezea nguvu sheria zinazohusiana na maandamano ya raia ili kupambana na mawazo ya siasa kali ya wanasiasa wa mrengo wa kulia. Muungano wa chama cha Social Democratic na chama cha Kijani umetishia kumhuku mtu yeyote kifungo cha miaka mitatu gerezani anayepinga, kutukuza au kuunga mkono mateso yaliyofanywa na manazi. Vyama vya upinzani vimelikaribisha pendekezo hilo, lakini vinataka swala hilo lijadiliwe kwa kirefu. Maandamano yaliyopangwa kufanyika mjini Berlin mwezi Mei chini ya uandalizi wa chama cha kitaifa cha Ujerumani, yalizusha mjadala kuhusu kupunguza haki ya kufanya mikutano ya hadhara. Maandamano ya manazi wa kileo mapema mwezi huu yalitatiza sherehe zilizofanyika mjini Dresden, za kukumbuka kushambuliwa kwa mji huo na jeshi la muungano wakati wa vita vya pili vya dunia.