BERLIN: Ujerumani yapongeza katiba Afghanistan
5 Januari 2004Matangazo
Serikali ya Ujerumani imeipongeza Afghanistan baada ya Baraza Kuu la Wazee wake wa jadi "Loya Jirga" kupasisha katiba mpya na kuitaja kuwa ni hatua muhimu katika juhudi za ujenzi mpya wa nchi hiyo. Waziri wa mambo ya nje Joschka FISCHER amesema kuwa katiba hiyo ni msingi wa maendeleo ya demokrasia na changamoto katika juhudi za kuimarisha mfumo wa kisiasa na kijamii nchini Afghanistan. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amewapongeza wajumbe hao wa Baraza la kutunga katiba kwa kusisitiza kanuni za kutetea haki za binadamu ndani ya katiba hiyo. Kwa upande wake, Waziri wa Ujerumani wa misaada ya maendeleo Heidemarie WIECZOREK-ZEUL amesisitiza kuwa harakati za ujenzi mpya wa Afghanistan bado zinahitaji ushirikiano mkubwa wa kimataifa ili kusaidia kuimarisha maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini humo. Itakumbukwa kuwa Ujerumani imekuwa msitari wa mbele katika juhudi hizo, ikiwa ni pamoja na kuchangia kikosi kikubwa katika jeshi la kimataifa la kulinda amani nchini Afghanistan, pamoja na mafunzo ya jeshi jipya la polisi. Disemba 2001, Ujerumani ilikuwa pia mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa makundi mbali mbali yaliokuwa yakizozana nchini Afghanistan, uliomalizika kwa kuteuliwa serikali ya mpito chini ya uongozi wa Rais wa sasa Hamid KARZAI.
Matangazo