BERLIN : Ujerumani yaitaka G8 isiipe msaada Sudan
3 Julai 2005Waziri mdogo wa mambo ya nje wa Ujerumani Kerstin Müller amesema kwamba kundi la mataifa manane yenye maendeleo ya viwanda duniani linapaswa kutoisamehe madeni na kutoipa msaada wa fedha wa kimataifa Sudan ili kuilazimisha serikali ya nchi hiyo kuboresha hali ya haki za binaadamu ambayo ni mbaya sana hususan katika jimbo la Dafur.
Müller amesema Ujerumani iko tayari kuongeza msaada wake wa kibinaadamu kwa Sudan iwapo serikali ya nchi hiyo itachukuwa hatua za kuleta demokrasia na kuendeleza utawala wa sheria.Watu wanaokadiriwa kufikia 180,000 wamekufa kutokana na mapigano,njaa na maradhi wakati wengine milioni mbili wamekimbia nyumba zao kuepuka kuuwawa na kubakwa.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ameonya kwamba bila ya kuigilia kati mzozo wa jimbo la Dafur nchini Sudan unaweza kuja kugeuka kuwa marudio ya mauaji ya halaiki ya Rwanda.
Onyo hilo ni taarifa kali kabisa ya Annan kuwahi kuitowa juu ya mgogoro huo.