BERLIN. Ujerumani kuongeza idadi ya majeshi yake nchini Afghanistan
12 Agosti 2005Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Peter Struck amesema kwamba anatilia maanani hatua ya kuongeza idadi ya wanajeshi wa Ujerumani Bundeswehr hadi wanajeshi 3000 nchini Afghanistan.
Amesema kwamba atatoa pendekezo lake hilo mbele ya baraza la mawaziri mwezi oktoba.
Ujerumani hadi sasa ina wanajeshi 2,200 nchini Afghanistan na waziri Struck amesema kuwa iwapo pendekezo lake litakubalika basi Ujerumani itaongezea eneo la huduma ya wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan hadi magharibi mwa nchi hiyo.
Jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan ni baadhi ya kikosi cha kulinda amani cha NATO.
Wakati huo huo katika siasa za Ujerumani bibi Angela Merkel wa chama cha upinzani cha CDU na mgombea wa kiti cha ukansela wa Ujerumani amejitenga na matamshi yaliyotolewa na kiongozi wa tawi la Bavaria la chama cha upinzani bwana Edmund Stoiber kwamba wapiga kura kutoka Ujerumani Mashariki wamepoteza muelekeo wa kisiasa.
Bibi Merkel alikiambia kituo cha televisheni cha taifa kwamba matamshi hayo ya bwana Stoiber ni ya kugawanya watu.
Hivi karibuni bibi Angela Merkel anatarajiwa kukutana na kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder wa chama SPD katika mjadala utakao fanyika tarehe 18 septemba.
Kura ya maoni ya kituo cha televisheni ya ZDF inaonyesha bibi Angela Merkel anaongoza kwa asilimia 41 dhidi ya kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder ambae ana asilimia 31.
Matokeo kamili yatategemea mchango wa vyama vidogo na chama kipya cha mlengo wa kushoto.