BERLIN : Ujerumani inasema jibu la Iran halitoshi
25 Agosti 2006Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema jibu la Iran kwa mpango wa vifuta jasho wenye nia ya kuishawishi Iran kusitisha shughuli zake nyeti za nuklea haliridhishi.
Akizungumza katika televisheni ya Ujerumani Merkel amesema jibu hilo la Iran limeshindwa kukidhi madai ya Umoja wa Mataifa yenye kuitaka nchi hiyo isitishe shughuli zake za kurutubisha uranium.
Ujerumani ni miongoni mwa mataifa sita makubwa ambayo yameipatia Iran mpango huo wa vifuta jasho vya kiuchumi na kisiasa. Nchi nyengine ni Marekani,Uingereza,Ufaransa,Urusi na China.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeipa Iran hadi tarehe 31 mwezi wa Augusti kusitisha mpango wake wa kurutubisha uranium au kukabiliwa na vikwazo vya kuiadhibu nchi hiyo.