BERLIN : Uchaguzi wa Ujerumani kuwa wa mchuano mkali
16 Septemba 2005Ikiwa zimebakia siku tatu kufanyika uchaguzi mkuu wa bunge nchini Ujerumani uchunguzi wa maoni unadokeza kwamba matokeo yatakuwa ya mchuano mkali.
Chama cha kihafidhina CDU kinaendelea kuongoza kwa pointi nane dhidi ya chama cha SPD cha Kansela Gerhard Schroeder.Lakini haiko dhahiri iwapo CDU na washirika wao inaopendelea kuunda nao serikali ya mseto chama cha FDP vitaweza kuwa na kura za kutosha kuwa na wingi wa viti bungeni na kuunda serikali.
Katika matukio ya karibuni kabisa kuhusiana na uchaguzi huo chama cha SPD kimekataa madai ya CDU kwamba waziri wake wa fedha Hains Eichel ana orodha ya siri ya punguzo la bajeti la thamani ya euro bilioni 30 iwapo serikali ya mseto ya mrengo wa shoto wa wastani ya Kansela Schroeder itarudishwa madarakani.
Msemaji wa SPD ameelezea madai hayo kuwa kampeni ya kupakana matope.