BERLIN: Sherehe za kuadhimisha mwisho wa Vita Vikuu vya Pili Duniani
7 Mei 2005
Sherehe za demokrasia zimefunguliwa katika mji mkuu Berlin nchini Ujerumani kuadhimisha mwaka wa 60 tangu Ujerumani ya Kinazi kusalimu amri.Sherehe hizo zimegubikwa na uwezekano kuwa siku ya Jumapili,Manazi mambo-leo wataandamana karibu na Lango la Brandenburg na kuzuka hatari ya kupambana na wana harakati wa siasa kali za kushoto.Polisi wamekaa tayari pindi kutazuka mapambano kati ya makundi hayo mawili.Wakati wa sherehe za demokrasia kutakuwepo maonyesho ya muziki wa vijana.Vile vile mishumaa inawashwa katika safu ya kilomita 30.Kwenye Lango la Brandenburg kumewekwa skrini kubwa kuonyesha hotuba zitakazotolewa siku ya Jumapili na Rais wa Ujerumani,Horst Köhler na Kansela Gerhard Schroeder.Kansela Schroeder baadae ataelekea Moscow nchini Russia kuhudhuria sherehe rasmi za kuadhimisha mwisho wa vita barani Ulaya miaka 60 ya nyuma.