BERLIN Rais wa Ujerumani ataka kukutana na viongozi wa upinzani
2 Juni 2005Rais wa Ujerumani, Horst Koehler amesema anataka kukutana na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani humu nchini kujadili mpango wa kuitisha uchaguzi wa mapema baadaye mwaka huu. Koehler lazima aamue ikiwa atalivunja bunge iwapo kansela Gerhard Schroeder atashindwa katika kura ya kutokuwa na imani na serikali yake bungeni hapo Julai mosi.
Rais Koehler anaweza kuukataa mpango huo na hivyo kuyadidimiza matarajio ya wengi kuhusu uchaguzi. Hivi karibu ameelezea kustaajabu kwake kwa kutohusishwa katika mpango huo wa kuitisha uchaguzi kabla wakati uliopangwa kufika.
Vyombo vya habari humu nchini vimekuwa vikihoji ikiwa mpango huo wa Schroeder unafuata katiba ya taifa. Waziri wa mambo ya ndani bwana Otto Schily, amesema mawaziri wanaweza kukataa kushiriki kupiga kura hiyo, hatua iliyotumiwa na kansela wa zamani Willy Brandt, iliyopelekea kuitishwa kwa uchaguzi wa mapema.