BERLIN: Raia wa Ujerumani kuachiliwa huru kutoka Guantanamo
24 Agosti 2006Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema nchi yake imefikia makubaliano na Marekani juu ya kuachiliwa huru mjerumani wa asili ya kituruki, Murat Kurnaz, aliyekuwa akizuiliwa katika jela ya Guantanamo.
Hata hivyo Steinmeier hakusema ni lini Kurnaz atakapoachiliwa huru.
´Kama mujuavyo makubaliano kati ya wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani na ofisi ya kansela yamefaulu baada ya majaribio kadhaa, chini ya ushirikiano na serikali ya Marekani, kumrejesha bwana Kurnaz nchini Ujerumani kutoka jela ya Guatanamo. Kesi yake ambayo ilisikilizwa mjini Washington na sasa imemalizika kwa ufanisi, ilisikilizwa chini ya uongozi wa ubalozi wa Ujerumani, lakini pia idara nyengine zilihusika ikiwemo wizara ya mambo ya ndani.´
Wanajeshi wa Marekani walimkamata Kurnaz mapema mwaka wa 2002 nchini Pakistan kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya kigaidi na wakampeleka Guantanamo Bay nchini Cuba.
Kurnaz ameyakanusha mashtaka yote dhidi yake.