BERLIN : Putin aunga mkono Ujerumani na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama
7 Mei 2005Matangazo
Rais Vladimir Putin wa Russia anasema anaunga mkono jaribio la Ujerumani kujipatia kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika mahojiano na gazeti la kila siku la Ujerumani la Bild Putin amesema Russia itaunga mkono Ujerumani kuwa na dhima madhubuti katika Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama.
Mahojiano ya pamoja na Putin na Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani yatachapishwa katika toleo la leo la gazeti hilo.
Viongozi hao wawili wanatarajiwa kuhudhuria kumbukumbu ya miaka 60 ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia mjini Moscow hapo Jumaatatu.