BERLIN: Njama ya kuripua bomu kwenye treni
19 Agosti 2006Nchini Ujerumani polisi wanasema mabomu mawili yaliyogunduliwa mwezi uliopita katika treni za abiria,huenda ikawa sehemu ya njama ya magaidi. Mabomu hayo yaligunduliwa pamoja na hati yenye maandishi ya Kiarabu kwenye treni katika miji ya Dortmund na Koblenz,tarehe 31 mwezi Julai.Mkuu wa idara ya uhalifu ya Ujerumani,Joerg Ziercke amesema,mabomu hayo yalipangwa kuripuka dakika 10 kabla ya treni kuwasili kwenye stesheni hizo mbili.Waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble amesema hakuna hakika kuwa kitisho kimemalizika. Polisi wameomba msaada wa umma kuwasaka watu 2 walio kati ya umri wa miaka 20 na 30.Wote wawili wameonekana katika picha zilizopigwa na kamera za ukaguzi kwenye stehseni ya treni ya mji wa Cologne,siku ambayo mabomu hayo yaligunduliwa.