Berlin. Mtuhumiwa wa ugaidi aachwa huru na mahakama nchini Ujerumani.
19 Julai 2005Mtuhumiwa mwanaharakati wa kundi la al Qaeda ameachwa huru kutoka jela nchini Ujerumani jana Jumatatu baada ya mahakama ya juu nchini humo kuzuwia mtu huyo kupelekwa nchini Uhispania.
Hispania inamshutumu mfanyabiashara huyo mzaliwa wa Syria anayeishi Ujerumani Mamoun Darkazanli kwa kutoa msaada wa fedha kwa mtandao wa kigaidi wa al Qaeda.
Darkazanli pia anaaminika kuwa na mahusiano ya karibu na wateka nyara wawili ambao walihusika katika mashambulizi ya hapo Septemba 11 nchini Marekani.
Lakini mahakama ya kikatiba ya Ujerumani imeamua kuwa kumpeleka Darkazanli nchini Hispania kwa kutumia hati mpya kukamatwa ya umoja wa Ulaya inakwenda kinyume na sheria ya msingi kwa kuwa hajapatikana na hatia ya uhalifu nchini Ujerumani.
Uamuzi huo wa mahakama umeshutumiwa na wanasiasa wa ndani na nje ya Ujerumani kuwa unarudisha nyuma mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.