BERLIN : Mkutano kutatuwa suala la Ukansela kufanyika leo
6 Oktoba 2005Vyama vikuu vya kisiasa nchini Ujerumani leo vinajiandaa kwa mkutano wa viongozi wenye lengo la kutafuta uvumbuzi wa mzozo wao wiki mbili na nusu juu ya nani anayepaswa kuiongoza nchi wakati chama cha wahafidhina cha Angela Merkel kikataraji kwamba Kansela Gerhard Schroeder atakubali kuuwachilia wadhifa huo.
Schroeder na Franz Muentefering mwenyekiti wa chama cha Schroeder cha SPD wanatazamiwa kukutana leo jioni na Merkel na kiongozi mwenzake wakihafidhina Edmund Stoiber.Viongozi hao wanne na washauri waandamizi walikutana hapo jana na kuonyesha kwamba wana mambo mengi wanayokubaliana katika suala la sera.
Tatizo kuu la mzozo huo bado kutatuliwa ambapo Schroeder na Merkel wote wawili wanadai kuwa na mamlaka ya kuwa Kansela.