Berlin. Merkel na Bush waiunga mkono Israel.
14 Julai 2006Rais wa Marekani George W. Bush na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wameyatetea mashambulizi ya Israel dhidi ya maeneo ya Lebanon, wakisema kuwa taifa hilo la Kiyahudi lina haki ya kujitetea dhidi ya maroketi ya wapiganaji wa Hizbollah.
Lakini viongozi hao wote Merkel na Bush wamesema kuwa Israel inapasha kuepuka kuidhoofisha serikali changa ya Lebanon.
Viongozi hao wawili walikuwa wanazungumza na waandishi wa habari kufuatia mazungumzo yao katika mji wa kitalii wa kaskazini mashariki ya Ujerumani katika bahari ya Baltic wa Stralsund, eneo la jimbo la anakotoka Bibi Merkel.
Mtazamo wao ulikuwa zaidi ukielekea kuipendelea Israel kuliko Ufaransa na Russia, ambazo zimeyaita mashambulizi ya Israel kuwa ni hatari kwa kuzidi kuchochea mzozo wa mashariki ya kati. Katika mazungumzo yao, Bush na Merkel pia walijadili mkwamo uliopo kuhusu nia ya Iran ya kujipatia teknolojia ya kinuklia.Viongozi hao wawili wanatarajiwa kusafiri kwenda St. Petersburg leo kwa mkutano wa mataifa tajiri ya G8 unaotayarishwa na Russia.