BERLIN: Merkel kutangaza Baraza la Mawaziri wake
17 Oktoba 2005
Baraza jipya la mawaziri wa Kansela-mteule wa Ujerumani,Bibi Angela Merkel,limekamilika.Kwa mujibu wa Naibu-Mwenyekiti wa chama cha CDU,Christian Wulff,mkuu wa chama cha CSU,Edmund Stoiber amekubaliana na Merkel kuwa naibu wake Horst Seehofer atakuwa waziri wa kilimo na hifadhi ya wanunuzi.Akaongezea kuwa mawaziri wengine wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU wameshateuliwa lakini hakutaka kuyataja majina yao.Hii leo,Bibi Merkel atatangaza majina ya mawaziri hao wapya.Baadae ndio yataanza majadiliano ya kuunda serikali ya muungano pamoja na chama cha Social Democrats-SPD ambacho tangu siku chache za nyuma kilitangaza majina ya mawaziri wake walioteuliwa.Vyama vya CDU,CSU na SPD vinatazamia kukamilisha majadiliano hayo hadi kati kati ya mwezi Novemba.