Berlin. Merkel atangaza baraza la mawaziri.
18 Oktoba 2005Kansela mtarajiwa nchini Ujerumani Angela Merkel ametangaza mawaziri wake kutoka chama chake cha kihafidhina ikiwa ni sehemu ya baraza lake la mawaziri akikamilisha orodha ya baraza la mawaziri katika serikali ya mseto.
Wolfgang Schäuble anakuwa waziri wa mambo ya ndani , na Franz Josef Jung anakuwa waziri wa ulinzi.
Edmund Stoiber , kiongozi wa chama ndugu cha Christian Social Union , alikwisha teuliwa hapo kabla kuwa waziri wa uchumi. Schäuble amekuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya hapo kabla kutoka mwaka 1989 hadi 1991 chini ya uongozi wa kansela wa zamani Helmut Kohl.
Katika makubaliano yaliyofikiwa wiki iliyopita kati ya chama cha CDU cha Merkel na kansela anayeondoka madarakani Gerhard Schröeder na chama chake cha Social Democrats, mawaziri wanane kati ya 14 watakuwa kutoka chama cha SPD kwa kukubali kuwa Merkel awe kansela mpya.
Mazungumzo katika kile kinachojulikana kama muungano mkuu kwa ajili ya serikali ya mseto yameanza siku ya Jumatatu na yanatarajiwa kuendelea hadi katikati ya mwezi Novemba.