BERLIN : Makubaliano ya kuunda serikali ya muungano mkuu yafikiwa
12 Novemba 2005Chama cha Christian Demokrat na kile cha Social Demokrat vimekamilisha makubaliano ya kuunda serikali ya mseto ya muungano mkuu.
Angela Merkel ametangaza kufikiwa kwa makubaliano hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin hapo jana. Makubaliano hayo yanakuja takriban miezi miwili kufuatia uchaguzi mkuu wa Ujerumani ulioshindwa kutowa mshindi dhahiri. Makubaliano hayo inabidi yaridhiwe na vyama hivyo ambavyo vinatarajiwa kukutana katika siku chache zijazo.Merkel sasa anatarajiwa kuchaguliwa kuwa Kansela wa kwanza wa kike wa Ujerumani katika kura itakayopigwa bungeni hapo tarehe 22 mwezi wa Novemba.
Maelezo kamili ya makubaliano hayo bado kutolewa lakini yanajulikana kujumuisha hatua za kupunguza nakisi inayoongezeka ya bajeti ya Ujerumani kwa euro bilioni 35.Pia imefahamika kwamba suala la kupunguza ukosefu wa ajira litakuwa jukumu kuu la sera za serikali.
Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini ambacho kinapindukia asilimia 10 kinaelezewa kuwa ni changamoto kuu inayoikabili Ujerumani.