Berlin. Majadiliano ya kuunda serikali ya mseto yanaendelea.
7 Novemba 2005Nchini Ujerumani , majadiliano ya kuunda serikali ya mseto katika kile kinachofahamika kuwa ni muungano mkuu yanaingia katika siku zake za mwisho.
Jana Jumapili vyama vikuu vya Ujerumani, chama cha kihafidhina na kile cha Social Democrats vilifanya mikutano yao tofauti wakijadili masuala muhimu katika sekta ya afya, soko la kazi na sera ya kodi.
Makubaliano yanatarajiwa kabla ya mwisho wa wiki hii.
Mpango wa kiongozi wa chama cha kihafidhina Angela Merkel wa kuongeza kodi ya ongezeko la bei VAT, ili kulipia gharama za punguzo la mishahara ulikosolewa vikali na viongozi wa chama cha Social Democrats katika kampeni za hivi karibu za uchaguzi mkuu na suala hilo ni moja kati ya linaloleta utata katika mazungumzo ya vyama hivyo. Siku ya Jumamosi, chama cha SPD kilionya kuwa kupandisha kiwango cha VAT kunaweza kuathiri matumaini ya ukuaji wa uchumi wa Ujerumani.