Berlin. Madaktari wafanya uchunguzi katika bata waliokufa.
26 Oktoba 2005Madaktari wa wanyama nchini Ujerumani bado wanafanya uchunguzi katika bata mzinga na bata wa kawaida 20 waliopatikana wamekufa katika Ziwa ili kuweza kufahamu iwapo wamekufa kutokana na mafua ya ndege.
Ndege hao walikutwa katika Ziwa linalotumiwa na ndege wanaohama hama katika jimbo la magharibi la Rhineland-Palatinate.
Mkuu wa ofisi inayofanya uchunguzi huo imesema kuwa hakuna dalili hadi sasa zinazoonyesha kuwa ndege hao wameambukizwa virusi vya mafua ya ndege. Lakini ameongeza kuwa uchunguzi zaidi unafanyika katika juhudi za kupata uhakika kuwa virusi vya H5N1 vya mafua ya ndege, ambavyo vinaweza kuwa hatari kwa binadamu havihusiki na vifo hivyo.
Wakati huo huo mataifa ya Afrika yanaendelea kupiga marufuku uingizaji wa nyama ya mifugo ya kuku na bata na kuimarisha uchunguzi wa ndege mwitu kutokana na hatari inayoendelea kuwa kubwa ya kuzuka kwa homa hatari ya mafua ya ndege katika bara hilo.
Katika muda wa wiki moja iliyopita kiasi cha mataifa zaidi ya 12 ya Afrika ambako wataalamu wanaamini ugonjwa huo unaweza kusambaa kutokana na kuwasili kwa ndege wanaohama hama kutoka Ulaya na bara la Asia wamepiga marufuku kabisa ama kwa kiasi fulani uingizaji wa kuku ama bata ama bidhaa zitokanazo na mifugo hiyo. Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, pamoja na mataifa kadha ya Afrika magharibi ya Togo na Sierra Leone ni baadhi ya mataifa yaliyojiunga na hatua hiyo hivi karibuni.