BERLIN. Ludger Volmer ashuhudia kuhusu kashfa ya visa mbele ya kamati ya bunge.
21 Aprili 2005Matangazo
Makamu waziri wa mambo ya kigeni wa zamani wa Ujerumani, Ludger Volmer, ameshuhudia mbele ya kamati ya bunge inayochunguza kashfa ya utoaji visa. Inasemekana kashfa hii iliwasaidia wahalifu na wahamiaji haramu kutoka Ulaya mashariki kuingia Ujerumani, na kukitia mchanga kitumbua cha waziri wa mambo ya kigeni, Joschka Fischer.
Volmer ameutetea mpango wa serikali ya Gerhard Schröeder kulegeza kamba sheria za utoaji visa mwaka wa 2000. Amesema sheria za zamani ziliwakandamiza raia wa kigeni. Kusikilizwa kwa ushahidi huo leo hii kulionyeshwa kwa mara ya kwanza katika runinga hapa nchini. Upinzani hata hivyo umeshikilia msimamo wake wa kumlaumu mwanasiasa huyo kwa kuwafungulia milango wahamiaji haramu.