Berlin. Kansela wa Ujerumani apanga kushindwa kwa hoja ya kuwa na imani naye bungeni.
1 Julai 2005Kansela wa Ujerumani Bwana Gerhard Schröder anatarajiwa kuwataka wanachama wa chama chake cha Social Democrats na chama shirika katika serikali cha Greens kutopiga kura katika kura ya kutokuwa na imani leo Ijumaa.
Hoja hiyo ina lengo la kulazimisha uchaguzi wa mapema nchini Ujerumani hapo mwezi wa Septemba.
Bwana Schröder alilishangaza taifa hapo May 22 wakati alipotangaza mipango ya kufanyika uchaguzi mkuu na mapema , mwaka mmoja kabla ya wakati wake, baada ya kushindwa vibaya chama chake katika uchaguzi wa jimbo kubwa nchini Ujerumani la North Rhine Westphalia.
Maelezo ya Bwana Schröder ya kutaka uchaguzi na mapema ni kwamba serikali yake haina tena uungwaji mkono wa bunge ambao ni muhimu katika kusukuma sera zake. Kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa , rais Horst Köhler atalivunja bunge katika muda wa siku 24 na kuamuru uchaguzi ufanyike , huenda hapo Septemba 18.