BERLIN: Kansela wa Ujerumani aitisha uchaguzi mapema
24 Mei 2005
Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani yadhihirika kuwa atakabiliana na kiongozi wa kihafidhina Bibi Angela Merkel kati kati ya mwezi wa Septemba,baada ya kuamua kuitisha uchaguzi mkuu mwaka mmoja mapema.Tarehe mosi Julai,Kansela Schroeder,atachukua hatua rasmi kuambatana na katiba ya nchi ya kulitaka bunge lipige kura ya kutokuwa na imani na serikali.Kwa mujibu wa katiba ya Ujerumani,serikali lazima ishindwe kura ya imani bungeni,ili iweze kuitisha uchaguzi, kabla ya wakati wake.Pindi serikali itashindwa bungeni,basi rais Horst Köhler ataweza kulivunja bunge na kupanga tarehe ya uchaguzi.Inatazamiwa kuwa uchaguzi mkuu utafanywa Septemba 18 baada ya kumalizika likizo za shule za majira ya joto.Kansela Schroeder alitangaza pendekezo la kuitisha uchaguzi mkuu mapema kuliko vile ilivyopangwa,muda mfupi tu baada ya chama chake cha SPD kushindwa vibaya kabisa katika uchaguzi muhimu wa jimbo la North Rhine Westphalia lenye wakaazi wengi kabisa na lililokuwa likitawaliwa na SPD kwa miaka 39.