BERLIN : Kampeni ya uchaguzi yazidi kupamba moto
17 Septemba 2005Wanasiasa wa Ujerumani wanaachana na utaratibu wao wa kawaida na badala yake wataendelea na kampeni hadi ya siku ya uchaguzi mkuu wenyewe hapo kesho Jumapili.
Kupamba moto huko kwa kampeni ya uchaguzi kunakuja wakati uchunguzi wa maoni ukionyesha kwamba takriban asilimia 25 ya wapiga kura bado hawakuamuwa nani wa kumpa kura zao. Uchunguzi tafauti wa maoni uliotolewa hivi punde tu umedokeza kwamba chama cha kihafidhina cha CDU pamoja na washirika wao inopendelea kuunda nao serikali ya mseto chama cha kiliberali cha Free Demokrat vinaweza kujipatia ushindi wa viti vichache bungeni.
Kansela Gerhrad Schroeder ameanza kampeni ya lala salama ya mwishoni mwa juma hapo jana kwa mkutano wa hadhara mjini Berlin ambapo ameishutumu mipango ya mageuzi ya kiuchumi ya CDU kwa kusema kwamba itakuja kusababisha mgawanyiko mkubwa katika jami kati ya wale wenye nacho na walala hoi.
Pia mjini Berlin mpizani wake wa chama cha CDU Angela Merkel ameuambia mkutano wa hadhara wa chama hicho kwamba serikali ya mseto ya mrengo wa shoto wa wastani ya Kansela Schroeder imeshindwa kutimiza ahadi zake tokea iingie madarakani miaka saba iliopita.