Berlin. Hali ya Uzbekistan inatia wasi wasi asema waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani.
15 Mei 2005Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Joschka Fischer ameeleza wasi wake mkubwa kuhusiana na matukio ambayo yamejitokeza nchini Uzbekistan. Katika taarifa yake iliyotolewa na wizara ya mambo ya kigeni mjini Berlin, Bwana Fischer amesema kila hatua inayowezekana inapaswa kuchukuliwa kuzuwia hali kuwa mbaya zaidi katika nchi hiyo.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Peter Struck amewaambia waandishi wa habari kuwa wanajeshi 300 wa Ujerumani walioko Uzbekistan hawako katika hali ya hatari, kwa kuwa kituo chao kiko kilometa 900 kutoka katika mji uliokumbwa na ghasia wa Andijan. Marekani imezitaka pande zote kuwa watulivu. Russia imeeleza wasi wasi wake kwa kile inachokieleza kuwa ni kitisho dhidi ya uimara katika jimbo hilo la zamani la Urusi.