Berlin. Greens wakutana kuidhinisha ilani ya uchaguzi.
9 Julai 2005Mkutano wa chama cha Green nchini Ujerumani unaofanyika mjini Berlin ulioitishwa kuidhinisha ilani ya uchaguzi , kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, ulianza kwa wajumbe kukaa kimya kwa muda wa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa shambulio la bomu mjini London.
Mgombea wa chama hicho cha Green , Bwana Joschka Fischer, amewataka wajumbe wa chama hicho kupambana ili kushinda katika uchaguzi mkuu ujao hapo Septemba 18, kwa misingi ya maadili ya chama hicho ya haki ya raia , ikiwa ni hapa nchini pamoja na nje.
Kutokana na mashambulio ya kigaidi mjini London , ambayo aliyaelezea kuwa ni kitendo cha ugaidi wa kidikteta, amesema Ujerumani ni lazima ikumbatie na sio kutupilia mbali, uhusiano wa tamaduni mbali mbali.
Kuiweka Uturuki nje ya umoja wa Ulaya kama inavyopendekezwa na chama cha upinzani cha kihafidhina, itakuwa ni hatua ya hatari itakayowatia moyo watu wenye imani kali za kidini.
Kuhusiana na masuala ya hapa nchini , Bwana Fischer amesema kuwa chama cha Green kitapendekeza sheria ya lazima ya kuwalea watoto wadogo, ili kuhakikisha kuwa akina mama wanarejea kazini.