BERLIN: Gaidi wa zamani aachiliwa huru
23 Desemba 2003Matangazo
Mahakama nchini Ujerumani imemwachilia huru gaidi mmoja maarufu wa zamani Hans-Joachim KLEIN aliyehukumiwa kifungo cha miaka 9 gerezani mwaka wa 2001 kwa mauaji ya watu 3. Mtu huyo alikatiwa pia kesi hiyo baada ya kukiri kuwa na nia ya kuuwa watu wengine 3 wakati wa mkutano wa mawaziri wa Jumuia ya nchi zinazochimba mafuta kwa wingi ulimwenguni OPEC mwaka wa 1975 mjini Vienna. Wizara ya sheria katika jimbo la Ujerumani la Hesse imesema kuwa mtu huyo ameachiwa baada ya maombi ya raia wengi mbali mbali ambao majina yao yamehifadhiwa. Kesi yake ilizusha hamasa kubwa miongoni mwa raia wa Ujerumani hasa baada ya kumhusisha Waziri wa sasa wa mambo ya nchi za nje aliyetakiwa kutoa ushahidi. Bwana Joschka FISCHER aliwahi kumfahamu KLEIN wakati wa ujana wake alipokuwa miongoni mwa wanaharakati wa mrengo wa kushoto kati ya miaka ya 1960s na 70s. Bwana KLEIN alikiri kuhusika katika shambulio dhidi ya kikao cha mawaziri wa OPEC lakini alikana kuhusishwa na mauaji yoyote.