BERLIN : Fischer aliomba ushauri juu ya kujiuzulu
5 Machi 2005Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Yoschka Fischer ambaye alikuwa akikabiliwa na wito wa upinzani wa kumtaka ajiuzulu kutokana na kashfa ya viza amekiri katika mahojiano na gazeti hapo jana kwamba alitafuta ushauri iwapo ajiuzulu au la.
Kamati ya bunge inaichunguza wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani kwa uzembe juu ya sera ya viza ambapo wapinzani wa kisiasa wanasema umewezesha magenge ya uhalifu ya Ukraine kuwaingiza nchini Ujerumani maelfu ya wahamiaji wasio halali wakiwemo wanawake wanaolazimishwa kuingia katika ukahaba.
Kashfa hiyo pamoja na ongezeko la ukosefu wa ajira kupindukia watu milioni tano vimetowa pigo kwa serikali ya mseto ya chama tawala cha Kansela Gerhard Schroeder SPD na kile cha Kijani cha Fischer katika uchunguzi wa maoni pamoja na kumharibia hadhi yake Fischer akiwa kama mwanasiasa aliye mashuhuri kabisa nchini Ujerumani.